Waefeso 4:15-16 - 23-06-2026

Date
Reading
Waefeso 4:15-16

Jumanne asubuhi tarehe 23.06.2026

Waefeso 4:15-16
15 Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo.

16 Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadiri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo.

Pamoja tujenge Kanisa la Bwana;
Mtume Paulo anawaandikia watu wa Efeso akiwasihi kuwa na umoja katika Kristo. Anasema umoja katika Kristo ni Agizo la Mungu mwenyewe katikati ya ushirika wa waaminio. Anawataka kuwa wapole, wavumilivu, wanaochukuliana kwa upendo, na kuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani. 
Angalia Paulo anavyoandika juu ya umoja katika Kristo;

Waefeso 4:4-6

4 Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.
5 Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja.
6 Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote.
Somo tulilosoma ni mwendelezo wa utangulizi hapo juu, Paulo akihimiza kuishika kweli katika upendo ili kumfikia Kristo. Paulo anasisitiza kuungana pamoja kwa mfano wa viungo vya mwili, tukijengana katika upendo utokao kwa Kristo mwenyewe. Ni kwa njia hiyo tunaweza kulijenga Kanisa la Bwana kwa pamoja. Amina
Siku njema

Heri Buberwa